Mambo usiyofahamu kuhusu mkoa wa Mtwara

UTANGULIZI

Mfumo wa utawala wa ukoloni uliigawa Tanzania katika Majimbo 8, Mkoa wa Mtwara ulikuwa ndani ya Jimbo la Kusini ambalo lilijumuisha Mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara ambapo Makao Makuu ya Jimbo yalikuwa Lindi.

Mkoa wa Mtwara ulianzishwa rasmi mwaka 1971 kutokana na Mpango wa Madaraka Mikoani ulioasisiwa na kusimamiwa na Rais wa Tanzania kipindi hicho ndugu Julius .K. Nyerere ambao ulilenga kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

Historia ya Mtwara inakuja sambamba na kumbukumbu la jaribio la Waingereza la kuanzisha mradi mkubwa wa maendeleo katika eneo hili ulioshindikana kabisa.

Kuanzia mwaka 1947 serikali ya kikoloni ilijenga bandari ya Mtwara pamoja na reli. Vilevile Mtwara mjini ilipangwa vizuri na kubwa. Sababu yake ilikuwa mpango wa kuanzisha kilimo cha mashamba makubwa kwa ajili ya karanga hasa zilizohitajika kwa ajili ya mahitaji ya Waingereza ya mafuta ya kupikia.

Mradi huo ulishindikana kabisa, pesa nyingi zilipotea hadi mradi ulifutwa kabla ya Tanzania kupata uhuru. Reli iliondolewa tena mwaka 1963.

Bandari imebaki ambayo haijaona kazi nyingi lakini bado ina faida ya kuwa na nafasi nzuri sana ya kupokea meli kubwa. Wakati wa mapambano dhidi ya serikali ya ubaguzi wa rangi katika Afrika Kusini mipango mbalimbali ilitungwa kutengeneza njia ya kupeleka bidhaa kutoka bandari ya Mtwara kwenda Songea na kutoka huko Malawi kwa kuvuka Ziwa Nyasa.

Baada ya kujengwa kwa daraja juu ya mto Rufiji mwaka 2002 kuna matumaini mpya ya kuwa na barabara inayotumika kati ya Mtwara na Dar es Salaam.

Eneo la Mnazi Bay ina gesi inayoweza kutumika kwa mahitaji ya nishati ya eneo lote.

Mkoa huu ulipoanzishwa ulikuwa tayari na Wilaya tatu (3) ambazo ni Masasi iliyoanzishwa mwaka 1928 chini ya ukoloni wa Kijerumani, Newala iliyoanzishwa mwaka 1956 chini ya wakoloni wa Kiingereza na Mtwara ilianzishwa mwaka 1961. Mahitaji muhimu kwa maisha ya geto

Kutokana na ongezeko la watu na kukua kwa Mkoa wa Mtwara ziliongezeka Wilaya nyingine 2 ambazo ni Wilaya ya Tandahimba iliyoanzishwa mwaka 1995 kutoka kwenye Wilaya ya Newala na wilaya ya Nanyumbu ilianzishwa
mwaka 2006 kutoka Wilaya ya Masasi.

Kiutawala Mkoa umegawanyika katika Wilaya 5 na Halmashauri 8, Tarafa 25, Kata zaidi ya 159, Vijiji 738, Vitongoji zaidi ya 3,126 na Mitaa isiyopungua 90. Aidha, Mkoa una halmashauri Tatu(3) za mamlaka ya miji  ambayo ni halmashauri ya Mji wa Mtwara Mikindani, halmashauri ya mji wa Masasi na halmashauri ya mji wa Newala.

MAANA YA NENO MTWARA

Neno Mtwara limetokana na neno la lugha ya Kimakonde “kutwala” ikiwa na maana ya kuchukua (kunyakua) kitu chochote.
Mtwara ni Jina inalotumika kwa maana 3 tofuati zifuatazo:
• Mtwara jina la Mkoa.
• Mtwara jina la mji wa Makao Makuu ya Mkoa.
• Mtwara ni Wilaya na Makao Makuu ya Wilaya ambayo kiutawala ina Halmashauri 2, ambazo ni Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani na Halmashauri ya Mtwara.

Kutokana na sensa ya taifa watu na makazi ya mwaka 2012 Mkoa wa Mtwara ulikuwa na jumla ya watu millioni moja laki  Tatu na elfu ishirini na nne(1,324,000). Mkoa wa Mtwara una makabila makuu 3 ambayo ni Wamakonde wanaopatikana katika
Wilaya za Mtwara, Tandahimba na Newala, Wayao na Wamakua wanaopatikana katika Wilaya za Masasi na Nanyumbu. Kihistoria makabila haya, hapo awali yaliishi pamoja na makabila mengine kaskazini mwa mto Ruvuma. Makabila hayo yaliacha makazi yao na
kukimbilia Msumbiji kutokana na uvamizi na vita vya makabila kutoka kaskazini mwa Tanganyika. Katika kuishi Msumbiji matarajio yao ya kuishi kwa amani na utulivu yalitoweka kutokana na kuibuka kwa vita vya Wazulu. Vita hivyo vilisababisha makabila hayo kurudi ng’ambo ya mto Ruvuma yalikokuwa zamani. Baada ya kuvuka mto Ruvuma,
Wamakonde, Wayao na Wamakua walitafuta maficho hadi kufikia katika bonde la Mkatahumbo na Chitandi. Walitulia katika maeneo hayo ili kuondokana na wasiwasi wa
kukamatwa na Wazulu.

MAHALI MKOA WA MTWARA ULIPO

Mkoa huu upo Kusini kabisa mwa Tanzania. Kijiografia upo kati ya Longitudo 38° na 40° Mashariki ya Griniwichi, na kati ya Latitudo 10° 05”na 11° 25” kusini ya Ikweta, na una eneo
la Kilomita za mraba 16,720 ambayo ni sawa na asilimia 1.9 (1.9%) ya eneo la Tanzania Bara ambalo ni kilomita za mraba 885,987. Takribani asilimia 3.91 (hkt 65,450) ya eneo la Mkoa lipo chini ya hifadhi mbili za wanyama ambazo ni Msanjesi (hkt 44,425) na Lukwika/Lumesule (hkt 21,025).

Mkoa wa Mtwara kwa upande wa Kaskazini umepakana na Mkoa wa Lindi, upande wa Mashariki umepakana na Bahari ya Hindi, upande wa Kusini kuna Mto Ruvuma unaotenganisha Tanzania na Msumbiji, wakati upande wa Magharibi umepakana na Mkoa wa Ruvuma.

HALI YA HEWA

Mkoa wa Mtwara una vipindi viwili vikuu vya majira. Majira ya mvua ambayo huitwa masika na majira ya ukavu ambayo huitwa kiangazi. Hakuna mvua za msimu maalum kama vile za Vuli zinazopatikana sehemu nyingine Tanzania. Kwa kawaida Mkoa wa Mtwara hupata mvua ya wastani wa mm 935 hadi 1,166 kwa mwaka. Wilaya inayoongoza kupata mvua nyingi ni Newala ambayo hupata wastani wa mm.1001, Wilaya inayopata mvua kidogo ni Nanyumbu ambayo hupata wastani wa mm.832.
Kwa kawaida kiwango cha juu cha joto Mkoani Mtwara ni 32C mwezi Disemba na kiwango cha chini cha joto huwa ni 28C mwezi Julai.

KABILA NA UTAMADUNI WA WAKAZI.

Asilimia kubwa ya Wakazi wa asili wa eneo hili ni wamakonde ambao wanatumia lugha ya kimakonde kama nyenzo ya mawasiliano, katika jamii ya kimakonde wamegawanyika katika sehemu mbili, sehemu ya kwanza ni wale wanaoishi katika Ukanda wa Pwani wanajulikana kama ”Wamalaba” na wale wanaoishi tofauti na ukanda wa pwani ” wamakonde wa bara” ingawa wanaongea lugha moja lakini kuna baadhi ya tofauti katika mfumo wao mzima wa maisha katika shughuli za kiuchumi, kijamii na desturi zao. Ukitaka kushuhudia haya unaweza kutembelea maeneo ya pwani kama vile Msangamkuu, Mgao, Nalingu, Msimbati na maeneo mengine yenye asili ya Pwani ambapo utakutana na vitu tofauti na sehemu za bara kama vile Mbawala, Kitere, Dihimba, Nanguruwe pamoja na sehemu zingine za Mtwara Vijijini.

SHUGHULI ZA KIUCHUMI.

Shughuli kuu za kiuchumi kwa wakazi wa eneo hili ni Kilimo kwa wakazi wengi wa Bara, Uvuvi kwa wakazi wanaoishi ukanda wa pwani na Ufugaji kwa kiasi kidogo kinafanywa na wananchi kutoka sehemu zote yaani bara na pwani. Zao kuu la biaashara ni korosho likifuatiwa na muhogo, Uvuvi na ufugaji wa kuku na mbuzi nao ni sehemu ya vyanzo vya kipato cha wakazi wa eneo hili hadi sasa

AINA YA UDONGO

Udongo hutegemea hali ya jiolojia. Katika Mkoa huu kuna kanda mbili za kijiolojia. Kwanza ni ukanda wa pwani ambao unaendelea kwa kilomita 125 kutoka bahari ya Hindi hadi ukanda
wa Makonde ujulikanao kama Makonde plateau uliopo Newala. Ukanda huu udongo wake ni wa kichanga na wenye rutuba hafifu na uwezo mdogo wa kushikilia maji. Maeneo mengine katika ukanda huu yana udongo mzito
wa aina ya mfinyanzi. Vilevile mawe ya chokaaa yaliyopo pwani hutoa udongo mwekundu unaopitisha maji vizuri.
Ukanda wa pili wa kijioliojia huendelea Magharibi ya ukanda wa pwani, ukanda huu una asili ya mawe yaliojishindilia kwa chini. Kaskazini ya mji wa Masasi kuna udongo wa mfinyanzi uliochangayika na udongo mwekundu, udongo huu ndio bora kuliko aina zote kwani ndio unaofaa kwa mazao ya chakula na biashara.

Like page yetu Facebook

Related Posts

Msomeni Blogu

Najihusisha na masuala ya kimtandao, mbinu mbalimbali za kuanzisha na kuendeleza biashara ya mtandaoni. Email yangu ni msomeniblogu@gmail.com au WhatsApp namba ni 0718453258

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

© 2021 MSOMENI BLOG - Theme by WPEnjoy · Powered by WordPress